Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Muhammad Abdu, Kaimu Mkurugenzi wa Hawza ya Imaam Swa’adiq (as), aliyasema hayo katika kipindi maalum kilichorushwa hewani kupitia Swa’adiq Media, Sheikh Muhammad alisisitiza kuwa; uongozi siyo tu mamlaka, bali ni dhamana inayohitaji ukaribu na huruma, alishauri viongozi wajipangie siku maalumu, iwe ni mara moja kwa mwezi au kila baada ya miezi miwili, ili kusikiliza malalamiko na matakwa ya raia wanao waongoza moja kwa moja, bila vikwazo au kupitia kwa watu wengine (mlolongo wa watendaji).
Alisisitiza kwa kusema: "Ni wajibu wa kimaadili kwa kila kiongozi—kuanzia ngazi ya Udiwani, Umeya, Ubunge, na hadi Uwaziri—kufungua milango ya ofisi zao na kusikiliza vilio vya wananchi ndani ya himaya zao."
Katika kuimarisha wito wake, Sheikh Muhammad alinukuu hekima nzito ya Kiongozi wa Waumini, Ali ibn Abi Talib (as), katika barua yake ya 67 aliyomwandikia Gavana wake wa Makkah wakati huo, Quthum ibn Al-Abbas:
وَ لَا تَحْجُبَنَّ ذَا حَاجَةٍ عَنْ لِقَائِكَ بِهَا فَإِنَّهَا إِنْ ذِيدَتْ عَنْ أَبْوَابِكَ فِي أَوَّلِ وِرْدِهَا لَمْ تُحْمَدْ فِيمَا بَعْدُ عَلَى قَضَائِهَا
"Wala usimzuilie mwenye haja asiufikie mkono wako kwa ajili ya haja yake; kwani yeye akizuiwa mlangoni pako tangu mara ya kwanza (alipokuja), basi hatoona sifa (hatafurahia) baadaye utakapomtimizia ile haja."
Akifafanua hekima hiyo, Sheikh Muhammad alibainisha kuwa; mojawapo ya dosari kubwa inayomomonyoa uaminifu kwa viongozi leo hii, ni kuweka vizuizi (kuta) vinavyozuia raia kuwafikia wanapokuwa na shida, tabia hii inajenga tabaka hatari kati ya kiongozi na anaowaongoza.
"Kiongozi unaposhindwa kuwasiliana na raia wako moja kwa moja fahamu kuwa umepoteza sifa ya uongozi bora, kumbuka watu wako wa karibu mara nyingi ni vigumu kukuambia ukweli, kwani hukuambia yale tu yatakayokufurahisha ili wabaki karibu nawe, lakini utakapofungua milango ya kusikiliza moja kwa moja, utajifunza ukweli mchungu na mambo mengi ambayo hukuyatarajia, na hayo ndiyo yatakayokusaidia kufanya maamuzi sahihi," alisisitiza Sheikh Muhammad.
Aliongeza kuwa, Imam Ali (as) anatufundisha somo ambalo viongozi wengi wamelipuuza au kuliacha. "Leo hii, mwananchi anapokujia na haja yake, ukimrejesha mara kadhaa kwa dharau, hata ukija kumtimizia haja hiyo baadaye, hawezi kukuona wewe kama kiongozi anayemjali, bali utabakia na doa la dharau uliyomwonesha awali. Ni wakati wa kushikamana na wosia huu mzito wa Imam Ali (as), kwani wengi tunakosea bila kujua, kwa sababu tu ya kuweka uzio kati yetu na raia tunaowaongoza."
Katika kuhitimisha hotuba yake, Sheikh Muhammad Abdu alihimiza umuhimu wa unyenyekevu huku akisisitiza kwa kusema: "Suala la uongozi ni jambo la mpito tu; wala lisiwe sababu ya kututenganisha na ubinadamu na uhalisia wa maisha, tusiache madaraka yatufanye tujisahau na kupoteza utu wetu, hii ndiyo nukta muhimu sana ambayo Imam Ali (as) aliisisitiza, nami ningependa kuiashiria kama ujumbe wa msingi katika Hijja ya mwaka huu."
Maoni yako